This post is also available in: English Español (Spanish) Français (French) 简体中文 (Chinese (Simplified)) 繁體中文 (Chinese (Traditional)) العربية (Arabic) Русский (Russian) Deutsch (German) Português (Portuguese, Portugal)
KANUNI ZA MAADILI NA DESTURI ZA KITAALUMA ZA SHIRIKA LA DUNIA LA UTAFITI WA MAONI YA UMMA (WAPOR)
Ilipitishwa Septemba 17, 2021
Note: This document was translated from English into many different languages. In case of any discrepancy or inconsistency between the English version and any other translation, the English version shall always prevail.
I. DIBAJI
A. WAPOR ilisasisha kwa mara ya mwisho Kanuni zake za Maadili na Desturi za Kitaalamu (kuanzia hapa na kuendelea tutaiita Kanuni) mwaka wa 2011 na ulimwengu wa utafiti, hasa utafiti wa maoni ya umma, umekuwa na mabadiliko mengi katika teknolojia ya ukusanyaji wa data, kushirikishwa kwa umma kwenye utafiti, tetezi zinazoongezeka kuhusu faragha ya data ya kibinafsi, mazingira ya uendeshaji wa chaguzi za kisiasa katika nchi nyingi, kuongezeka kwa zana mpya kama vile paneli za mitandaoni na matumizi ya matokeo ya utafiti kwa vyombo vya habari na vinginevyo.
B. WAPOR imesasisha Kanuni zake ili zilingane na mabadiliko haya na kutoa viwango bora kwa wanachama wake. Tumekagua Kanuni za Maadili zilizosasishwa hivi karibuni za AAPOR (Shirika la Marekani la Utafiti wa Maoni ya Umma, 2021) na kanuni za kimataifa za ICC/ESOMAR (2016).Tunaamini kuwa kanuni za 2021 za WAPOR zinalingana na viwango vya kitaaluma vya mashirika yetu huku tukizingatia mahitaji ya wanachama wa WAPOR, ambao wengi wao wanafanya utafiti wa kitaalam.
II. UTANGULIZI
A. Shirika la Dunia la utafiti wa maoni ya umma (WAPOR) na wahusika wake wa kikanda, katika kutimiza lengo lake kuu la kuendeleza matumizi ya sayansi katika utafiti wa maoni ya umma na katika kutambua wajibu wake kwa umma, hapa inaeleza kanuni za maadili, desturi za kuwaongoza wanachama wake, na mfumo wa kitaaluma na wa viwango vya maadili vinavyopaswa kukubalika kwa wafadhili wa utafiti wa kisayansi na kwa umma kwa ujumla.
B. Kanuni za maadili za WAPOR zinatumika katika aina zote za tafiti zinazozingatia mada mahususi , ikiwa ni pamoja na, lakini si tu, ukusanyaji wa data kwa kuwahoji watu na kupitia uchunguzi (pasipo kuwahoji watu), matumizi ya mbinu zinazozingatia idadi na ubora katika utafiti; utafutaji wa data na mchanganyiko wa aina za data ikiwa ni pamoja na , lakini si tu, CAPI, CATI na CAWI. Viwango vya maadili vinatumika bila kujali vifaa au zana zitakazo tumika kukusanya data.
C. Katika dunia inayozidi kuwa changamani , mipango ya kijamii na kiuchumi inaendelea kutegemea maoni ya umma yanayokusanywa vyema. Umma kwa ujumla ni chanzo cha kiasi kikubwa cha taarifa hizi . Kwa hivyo wanachama wa WAPOR wanatambua kuwa wana wajibu wa kulinda umma kutokana na upotoshaji na unyanyasaji kwa jina la utafiti. Wakati huo huo , WAPOR inathibitisha uhusiano wa kutegemeana kati ya uhuru wa mtu kueleza maoni yake na uhuru wa mtafitikufanya utafiti wa maoni ya umma kwa madhumuni yote mawili ya kitaaluma na kibiashara.
D. Wanachama wa WAPOR wanatambua wajibu wao kwa taaluma waliyo nayo na kwa wale wanaowapa msaada kutekeleza taaluma hiyo ili wazingatie viwango vya msingi vya uchunguzi wa kisayansi na kutoa taarifa.
E. Kanuni hizi zinafafanua maadili na desturi za kitaalamu katika nyanja yautafiti wa maoni ya umma. Kuzingatia kanuni hizi kunachukuliwa kuwa swala muhimu ili kudumisha imani ya kuwa watafiti katika nyanja hii wanaongozwa na kanuni bora na za msingi ambazo zimekuzwa kwa msingi wa uzoefu uliopatikana kwa miaka mingi katika mataifa mengi.
F. Ingawa uanachama katika WAPOR hauhakikishi uzingatiaji wa Kanuni hizi au kiwango fulani cha ubora wa utafiti, wanachama wote wa WAPOR wamejitolea kufuata Kanuni hizi katika nyanja zote za kufanya utafiti na kuchapisha matokeo.
G. Kama sehemu ya kujitolea kwake kwa uweledi na maadili katika nyanja zote za utafiti, WAPOR itaendelea kufanya warsha juu ya masuala haya (kupitia mtandao na vikao kwenye mikutano ya mwaka/kikanda), itaendelea kufikia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii katika nchi zenye wanachama ili kuarifu vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu mabadiliko katika utafiti, viwango vinavyoendelea kukuzwa vya utoaji taarifa na kulinda faragha ya wahojiwa, na itaendelea kutoa miongozo mingine ya kuripoti utafiti.
III. FAFANUZI
A. Watafiti wanafafanuliwa kama watu binafsi, makampuni na mashirika yenye jukumu la kiutendaji la kuunda utaratibu wa tafiti,, ukusanyaji wa data na uchakataji, ,uchambuzi, na usambazaji wa data
B. Watu Wanaofanyiwa Utafiti ni chanzo cha data ya utafiti. Pia wanajulikana kama wahojiwa, washiriki, watafitiwa , na majina mengine. Watafitiwa kwa kawaida hushiriki kwa hiari ingawa katika miradi mingine huwa wanapewa fidia. Fidia haibadilishi majukumu ya mtafiti kwa wahojiwa.
C. Maelezo Tambulizi ya Kibinafsi (PI) ni pamoja na, lakini si tu maelezo kuhusu Mhojiwa: jina, mahali anapoishi (nyumbani, kazini kwake, anwani ya posta), nambari za simu (ya mezani na rununu), barua pepe, akaunti za mitandao ya kijamii, data kutoka kwa programu za kutuma ujumbe (kama vile Whatsapp), data ya GPS inayoweza kutambua mtu binafsi au boma yake, picha, sauti na rekodi za video, na namba za kitambulisho zilizotolewa na serikali.
D. Wafadhili/Wateja wanaweza kujumuisha watu binafsi, makampuni ya faida, mashirika ya hisani, serikali, na mashirika ya kimataifa ikiwa ni pamoja na, lakini si tu masharika yasiyo ya kiserikali (NGOs). Hawa wote wanafaa wazingatie Kanuni za Maadili za WAPOR ikiwa wanaidhinisha utafiti kwa ushirikiano na wanachama wa WAPOR.
E. Vyombo vya Habari vinajumuisha watu binafsi na mashirika ambayo yanaweza kuwasilisha data ya maoni ya umma katika vyombo vya kuchapisha habari (kwa njia ya karatasi au ya kieletroniki) na katika vyombo mbalimbali vya utangazaji. Kanuni za Maadili za WAPOR zinatumika pale ambapo data iliyokusanywa na wanachama wa WAPOR inachapishwa na Vyombo vya Habari.
F. Mitandao ya Kijamii ni majukwaa yanayosaidia watumiaji katika mawasiliano namwingiliano wa kubadilishana habari na maudhui ya vyombo vya habari kati ya watu binafsi na vikundi kupitia njia za kidijitali, kimahususi blogu maalum, vikao vya mtandaoni, jamii za mtandaoni na vituo vya mawasiliano. Mitandao ya kijamii au vituo vyake vinaainishwa kama vilivyo ‘wazi’ au vilivyo ‘fungwa.’
IV. VIWANGO VYA MAADILI KATIKA MAHUSIANO KATI YA WATAFITI NA WAFADHILI AU WATEJA
A. MAJUKUMU YA WATAFITI
1. Utafiti huru unaolenga ukweli na data, uliotekelezwa kwa usahihi kama inavyoruhusiwa na rasilimali na mbinu zilizopo, ni kanuni inayoongoza tafiti zote.
2. Mtafiti atatoa taarifa sahihi kwa wafadhili wanaotarjiwa kuhusu uzoefu wake, uwezo wake, na shirika lake.
3. Mtafiti atafanya kila juhudi katika kuzingatia masharti yaliyopendekezwa na kukubaliwa na mfadhli/mteja. Iwapo mtafiti ataona anahitaji kwenda kinyume cha masharti hayo , atahitaji kupata idhini ya awali ya mfadhili/mteja kabla ya kufanya hivyo.
4. Mtafiti hatachagua zana za ukusanyaji au uchambuzi wa data kwa sababu ya uwezekano kwamba zitaunga mkono hitimisho analotaka. Kila chombo kitachaguliwa kulingana na kufaa kwake kisayansi, ikizingatiwa kuwa huenda kukawa na vikwazo vya muda na bajeti katika tafiti za kibishara , za sekta ya umma, au za kitaalam.
5. Mtafiti katika kila ripoti na mawasilisho mengine ya matokeo atatofautisha kati ya mahitimisho aliyopata kwa msingi wa data na kile alichoona au kuhitimisha ambacho huenda kilitokana na ushahidi mwingine au imani na maadili ya kibinafsi.
6. Wakati wowote ambapo data kutoka kwenye utafiti mmoja inatolewa kwa zaidi ya mfadhili/mteja mmoja au wakati ambapo data inatolewa kwa wafadhili au wateja kadhaa, mtafiti atajulisha kila mfadhili/ mteja kuhusu jambo hilo. huu.
7. Wahojiwa watajulishwa kuhusu mfadhili au mteja wa utafiti kwa ombi lao, isipokuwa mtafiti na mfadhili au mteja wawe wanaamini kuwa hiyo inaweza kusababisha majibu yanayoegemea upande fulani. Katika hali kama hiyo na baada ya mhojiwa kuwasilisha ombi lake, wahojiwa wataambiwa mfadhili au mteja ni nani baada ya data kukusanywa.
8. Taarifa zote na nyenzo zinazotolewa na mfadhili au mteja wa utafiti zitabaki kuwa siri. Zitatumika tu katika muktadha huu na hazitapeanwa kwa wahusika wengine bila idhini ya awali ya mfadhili au mteja.
9. Bila idhini ya awali ya mfadhili au mteja, hakuna matokeo kutoka katika utafiti uliodhihinishwa yatafichuliwa na mtafiti isipokuwa kama ilivyotajwa katika sehemu ya IV.B.5.
10. Isipokuwa kwa msingi wa idhini ya wahusika wote , data haitauzwa au kuhamishwa na mfadhili au mtafiti kwa yeyote ambaye hakushiriki katika kutia saini mkataba hapo awali. Kama data itahamishwa kwa msingi wa idhini ya wahusika wote, hiyo itatekelezwa kwa namna itakayohakikisha watafitiwa hawatatambuliwa.
11. Isipokuwa kama kuna makubaliano kati ya mtafiti na mfadhili/mteja, mbinu za utafiti kama vile miundo ya sampuli, maagizo ya mhoji, miundo ya uthibitishaji, maneno ya dodoso, zana za uchambuzi n.k., vilivyotumika katika utafiti, vitabaki kama mali ya mtafiti ikiwa yeye ndiye aliyezibuni.
12. Isipokua kama kuna makubaliano baina ya mtafiti na mteja/mfadhili kinyume cha sharti hilo, data zote, nyaraka za utafiti (kama vile itifaki na dodoso) au nyenzo nyingine yoyote iliyotumika katika utafiti itakuwa mali ya mtafiti. Mtafiti hata hivyo anatakiwa kuhifadhi nyenzo hizo kwa muda wowote uliowekwa kisheria au unaotumika kwa kawaida katika nchi husika . Sharti hili litachukuliwa kuwa limetimizwa ikiwa nyenzo husika zitahifadhiwa katika hifadhidata inayotambuliwa, ikihitajika, iweze kufikiwa tu na watu waliodhinishwa.
13. Baada ya kukamilika kwa utafiti na baada ya mtafiti kuwasilisha ripoti ya mwisho, mfadhili/mteja anaweza kutoa ombi, kulingana na makubaliano ya awali kati ya wahusika wote, nakala nyingine ya seti ya data, mradi mfadhili atagharamia maandalizi ya nakala kama hizo, na waliohojiwa kubaki bila kutambuliwa.
B. MAJUKUMU YA WAFADHILI/ WATEJA
1. Wafadhili au wateja watarajiwa wanaoomba mapendekezo ya tafiti na gharama za utekelezaji wanatambua ya kwamba, ikiwa hakuna ada au aina nyingine ya malipo, mapendekezo ya tafiti na gharama za utekelezaji zinabaki kuwa mali ya mtafiti. WAPOR inatarajia kuwa wafadhili au wateja watarajiwa; (a) hawatatumia mapendekezo ya mtafiti mmoja kujadili punguzo la gharama ya utekelezaji na watafiti wengine na (b) hawatashiriki mali bunifu , mbinu, au mapendekezo ya mtafiti bila idhini yake.
2. Ripoti zinazotolewa na mtafiti kwa kawaida ni za matumizi ya mfadhili/mteja na mawakala wake . Mtafiti na mfadhili au mteja watakubaliana kuhusu mbinu za usambazaji wa matokeo kamili au sehemu ya matokeo ya utafiti kwa wahusika wengine au kwa umma.
3. Mteja au mfadhili na mtafiti watajiendesha kwa njia ya kujaribu kuhakikisha kwamba uchapishaji wowote wa matokeo ya utafiti hautawasilishwa, au kunukuliwa nje ya muktadha, au kwa namna inayopotosha ukweli au matokeo yoyote ya utafiti.
4. Mtafiti ataelezwa kuhusu namna ya uchapishaji utakaotumiwa na ni haki yake kukataa kutoa ruhusa kwa jina lake kunukuliwa kuhusiana na utafiti husika pale ambapo anaamini kuwa kifungu Cha IV.B.3 kimekiukwa.
5. Ikiwa mtafiti atagundua kuwa utafiti husika umejitokeza hadharani ukiwa na upotoshaji mkubwa, atafichua hadharani kinachohitajika ili kurekebisha upotoshaji huo, ikijumuisha kama inavyofaa, taarifa kwa vyombo vya habari au vikundi vingine ambapo matokeo hayo potovu yaliwasilishwa.
C. KANUNI ZA DESTURI KUHUSU RIPOTI NA MATOKEO YA UTAFITI
1. Every report on a study shall contain a complete and accurate description of the following relevant points: / Kila ripoti ya utafiti itakuwa na maelezo kamili na sahihi ya mambo muhimu yafuatayo:
(a) Wateja/Wafadhili walioomba utafiti utekelezwe, na vyanzo vya fedha ikiwa ni tofauti.
(b) Wakusanyaji wa Data waliofanya utafiti, na majina ya Mchakataji/Wachakataji wa Data , na Mhusika au Wahusika wanaotoa sampuli, ikiwa inahitajika.
(c) Madhumuni ya utafiti.
(d) Kundi la watu wanaolengwa na matokeo ya utafiti.
(e) Njia iliyotumiwa kuchagua sampuli , ikiwa ni pamoja na mbinu ya kuchagua sampuli (bahati nasibu, kuchagua kwa upendeleo,, kuchagua watu mahususi, kuchagua watu mtandaoni na kadhalika) taratibu maalum zilizotumiwa kuchagua sampuli, na ukubwa halisi wa sampuli, ikiwa ni pamoja na maelezo kuhusu kuchagua watu mahususi na kudumisha kushiriki kwao wao.
(f) Kiwango cha mafanikio katika kutengeneza vigezo vya sampuli na utekelezaji wa muundo wa sampuli, pamoja na kiwango cha kutojibu, jinsi kilivyohesabiwa, na ulinganisho wa ukubwa na sifa za sampuli halisi na inayotarajiwa.
(g) Maelezo ya taratibu za ukadiriaji (ikiwa zipo ) na/au taratibu zilizotumiwa kurekebisha data ambayo haijachambuliwa.
(h) Tarehe na mbinu za ukusanyaji wa data. Ukubwa wa sampuli kwa ujumla na ukubwa wa vikundi vidogo kama matokeo yao yanaripotiwa kando kando.
(i) Nakala ya kieletroniki ya dodoso kamili katika lugha zote zilizotumika kukusanya data, ikijumuisha maelekezo kwa wanaokusanya data.
(j) Ni matokeo yapi yatatokana na sehemu za sampuli (kwa mfano kwa kuchuja ), badala ya yale ya sampuli nzima.
(k) Mtafiti pia ataripoti mapungufu yoyote ya utafiti katika husisho ya idadi ya watu waliolengwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo, jiografia, hali za kimaeneo, hali zisizotarajiwa zinazolazimisha kutoendela na utafiti, hali ya hewa, majengo yasiyofikika, vurugu za kisiasa, masuala ya afya ya umma yasiyo bora, vikwazo vya data zilizokusanywa kutoka kwa mitandao ya kijamii (kama vile, lakini si tu kuondolewa kutoka kwenye Twitter) na vikwazo vya serikali dhidi ya tafiti za maoni.
(l) Hatua zilizochukuliwa ili kuhakikisha usahihi wa sampuli zitafafanuliwa kwa uwazi na kuwasilishwa.
(m) Watafiti watatoa maelezo sahihi ya matokeo ya utafiti ikiwa ni pamoja na, lakini si tu , makadirio ya makosa ya sampuli, athari za muundo, hesabu ya matokeo halisi, na athari ya hesabu (ngumu) za kubaini matokeo halisi ya utafiti.
(n) Baada ya matokeo ya utafiti kuripotiwa, kuchapishwa, au kutolewa kwa umma, watafiti wanapaswa kupeana nyenzo zifuatazo zinazoweza kupatikana na waombaji ndani ya siku 30 baada ya kuwasilisha ombi, chini ya sheria au vikwazo vyovyote vya kimkataba . WAPOR pia inatambua kuwa baadhi ya njia hizi zinamilikiwa na mtafiti au washirika wa nyanjani na ufichuzi unaweza kudhuru maslahi yao ya kibiashara. Bila shaka, nyenzo hizi zote zitafichuliwa kwa Mteja/Mfadhili wa utafiti.
(0) Taratibu za kudhibiti washiriki katika sampuli (kuchagua sampuli, mbinu za kuchagua washiriki katika sampuli, kutoa vichocheo, kuhifadhi data, kuwasilina upya na washiriki, kuandikisha washiriki wapya kutokana na wengine kujiondoa).
(p) Ikiwa inahitajika, maelezo ya jinsi wahoji walivyopewa mafunzo, kusimamiwa, na kufuatiliwa.
(q) Maelezo ya taratibu za ukaguzi wa wahojiwa ikiwa hazijaandikwa katika ripoti ya utafiti.
(r) Vielelezo vya kuona au vielelezo vingine (kadi za kuonyesha, picha, rekodi).
(s) Mbinu zilizotumika kupata ushirikiano wa wahojiwa, ikiwa ni pamoja na, lakini si tu , kuwapa vichocheo, mawasiliano ya mapema na ya kufuatilia baada ya kukataa kushiriki hapo awali.
(t) Taratibu zilizotekelezwa ili kuhakikisha ubora wa data, kwa kutumia programu za utafiti (CAPI, CATI, CAWI) au mawasiliano na watu (kupitia uchunguzi katika mahali pa utafiti na ukaguzi wa baadaye)
(u) Watafiti watatumia fomula za ubora za AAPOR-WAPOR kama zilivyoelezwa kwenye tovuti zao ili kufanya hesabu ya viwango vya Mawasiliano, Ushirikiano, Majibu, na Kukataa.
(v) Sampuli ambazo hazijafanyiwa hesabu za urekebishaji za vikundi vidogo ambavyo matokeo yake yameripotiwa.
(w) Maelezo ya uchambuzi wa kitakwimu wa data na fahirisi katika ripoti za utafiti ambayo yatatosha kusaidia katika utekelezaji wa tafiti zingine na watafiti huru.
2. Maneno ya kiufundi yatatumika katika ripoti kulingana na matumizi yao ya kawaida ya kisayansi.
V. VIWANGO VYA MAADILI KATIKA MAHUSIANO KATI YA WATAFITI NA WANAOTAFITIWA
1. Kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo ndani ya udhibiti wa mtafiti na mfadhili au mteja, hakuna mtafitiwa, mtoa taarifa, wahojiwa au washirika wengine wa utafiti wataathiriwa vibaya kwa sababu ya (a) majibu yao, ama (b) mchakato wowote wa utafiti (kama vile kukataa kushiriki). Mtafiti ataheshimu maamuzi ya mhojiwa kuhusu kushirika kwake katika utafiti na hatatumia mbinu yeyote ya kumfanya mhojiwa ajipate katika hali ambapo hawezi kutekeleza haki yake ya kujiondoa ama kukataa kupeana majibu katika awamu yoyote ya utafiti.
2. Watafiti wataheshimu haki za kisheria za watafitiwa katika utafiti kwa ajili ya faragha, usiri, na ulinzi wa data. Hii inatumika katika aina zote za taarifa tambulizi za kibinafsi zilizokusanywa kama sehemu ya mchakato wa utafiti na ambazo zinaweza kuhifadhiwa au kutohifadhiwa na mtafiti kwa kipindi kifupi kilichotangazwa . Taarifa hizo zinafafanuliwa katika sehemu ya III[2].
3. Hakuna jibu katika utafiti au matokeo ya utafiti yatahusishwa kwa njia yoyote na mhojiwa anayeweza kutambulika. Watafitiwa watabaki bila kutambulika isipokuwa katika hali nadra ambapo mhojiwa mwenyewe atapeana ruhusa ya kutambuliwa na ambapo kutambulika huko kunaruhusiwa na sheria. Mtafiti atachukua hatua za kuzuia ufichuzi wa mteja/mfadhili au watafiti wengine ambao wanaweza kupata data kutoka kwenye hifadhidata zinazoweza kufikiwa na umma kwa ujumla.
4. Njia ya mahojiano au njia nyingine yeyote itakayotumiwa na mtafiti haitatumika kamwe kama mbinu fiche ya kutimiza madhumuni mengine ikiwa ni pamoja na, lakini si tu , kutafuta soko ya bidhaa au huduma fulani, kutafuta mauzo, kutafuta fedha, au kampeni za kisiasa.
[1] https://www.icpsr.umich.edu/icpsrweb/content/DDR/disclosure.html
[2] https://www.icpsr.umich.edu/icpsrweb/content/DDR/disclosure.html
VI. VIWANGO VYA MAADILI KWA WAHOJI WALIOAJIRIWA NA WANACHAMA WA WAPOR
A. Kazi za utafiti na nyenzo zinazopokelewa, pamoja na taarifa zote kutoka kwa wahojiwa, zitawekwa siri na wahoji na hazitafichuliwa kwa yeyote aliye nje ya shirika linalofanya utafiti.
B. Hakuna taarifa iliyopatikana kupitia shughuli za utafiti itatumika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa faida ya kibinafsi au faida ya mhoji.
C. Utafiti utafanywa kwa kuzingatia kwa makini mwongozo wa utafiti kuhusiana na kuchagua sampuli ya utafiti, matumizi ya dodosa, na mawasiliano na mhojiwa. Hakuna mhoji atakayefanya zaidi ya utafiti mmoja akitumia wahojiwa wale wale isipokuwa hiyo iwe imeidhinishwa na shirika linaofanya utafiti na wateja wake.
D. Hakuna shinikizo kutoka nje, liwe la kisiasa au la kibiashara, litatumiwa na shirika la utafiti ili kuhalalisha ukiukaji wa Kanuni hizi.
E. Wanachama hawatajaribu kutumia uanachama wao katika WAPOR au uzingatiaji wao wa Kanuni hizi au Kanuni zingine zozote za Kimaadili kama ishara ya uwezo wao wa kitaaluma. Uanachama si hakikisho la utoshelezaji wa vigezo au uzingatiaji wa Kanuni hizi, lakini unamaanisha kwamba mwanachama husika amekubali Kanuni hizi.